ASEMA NI
BAADA YA KUBOMOA NYUMBA ZA VIGOGO
Happiness Mtweve, Dodoma-Tanzania daima
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Terezya Huvisa, amesema ametishiwa kuuawa endapo ataendelea
na zoezi la kubomoa nyumba za watu zilizo kwenye maeneo oevu.
Madai hayo aliyatoa jana mjini hapa,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema amepigiwa simu za
vitisho hivyo kwa lengo la kukwamisha jitihada zake za kuwashughulikia
wanaovunja sheria.
Alisema baada ya kupata vitisho
hivyo, aliamua kuwapigia simu lakini simu hizo hazikupatikana jambo
lililomfanya kuvipuuzia vitisho hivyo.
“Sijaviripoti polisi vitisho, najua
lengo lao lilikuwa kunitisha ili nisiendelee na mkakati wa kuwabomolea nyumba
wale waliojenga kwa kukiuka sheria, wanajidanganya nitaendelea kuwabomolea,”
alisema.
Alisema mtu yeyote mwenye jambo lenye
tija na masilahi kwa taifa kamwe asingesita kumpigia simu na ikiwezekana kwenda
kumuona juu ya bomoabomoa lakini waliompa vitisho hivyo ni ‘feki’.
Waziri huyo aliongeza kuwa
Mwanasheria la Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Heche Manchare,
naye alipewa vitisho pamoja na kupigwa na watu waliokuwa wamevalia vitambaa
usoni kwa lengo la kuficha sura zao.
Alibainisha kuwa tukio hilo
waliripoti kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ambaye aliwaambia
walifikishe polisi lifanyiwe uchunguzi zaidi.
Aliongeza kuwa pamoja na vitisho
hivyo kamwe wizara yake haitarudi nyuma katika zoezi la kuwabomolea nyumba,
hoteli au wawekezaji wowote wale waliojenga kwenye maeneo oevu.
“Hili ni zoezi gumu sana linalohitaji
ujasiri na umakini mkubwa sana, sisi hatutamuonea mtu yeyote, tumedhamiria
kufanya kazi zetu kwa nguvu hatarudi nyuma,” alisema.
Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya
Ndani, Emanuel Nchimbi, aliwataka viongozi na wananchi wote wanaopata vitisho
kuwasiliana na polisi ili hatua zichukuliwe.
Katika hatua nyingine, serikali
imeeleza kupata hasara ya sh bilioni 50 kwenye utekelezaji wa zoezi la
bomoabomoa katika fukwe za kawe na mbezi jijini Dar es Salaam.
Waziri Huvisa, alisema kuwa kiasi
hicho cha fedha ambacho serikali imekitumia ni kikubwa sana na kitalipwa na
wamiliki wa nyumba hizo ambao walijenga kinyume cha sheria na watazigawanya kwa
viwango mbalimbali kutokana na kila nyumba ilipokuwa imefikia.
Alisema kuwa wizaya yake
ilishirikiana na Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na Manispaa ya Kinondoni ambapo jumla ya nyumba saba na uzio nane
zilibomolewa na ujenzi uliokuwa unaendelea kwenye mkondo wa mto umebomolewa.
Alisema kuwa ubomoaji huu ni
utekelezaji wa sheria ya mwaka 2004 kutokana na wananchi hao kukaidi na
kutokutekelezwa kwa maagizo mbalimbali ya kutoendelea na ujenzi yaliyotolewa
kwa wahusika.
“Nawataka wale wote waliojenga na
wanaoendelea kujenga kwenye vyanzo vya maji, kando kando ya bahari, maziwa,
mito na mabwawa na misitu inayolindwa kisheria kuondoka mara moja na endapo
watakiuka maagizo hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema
waziri huyo.
Alifafanua kuwa hatua
zitakazochukuliwa dhidi yao moja wapo ni kuwabomolea nyumba zao na kuwaondoa
katika maeneo hayo na kwamba watatakiwa kulipia gharama zote zitakazohusu ubomoaji
huo.
Waziri alisema kuwa agizo
hilo pia linawahusu wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika vyanzo
vya maji
No comments:
Post a Comment